Waziri wa Utumishi wa Umma - Moses Kuria

Waziri wa Utumishi wa Umma nchini Moses Kuria ametoa ahadi ya kuboresha utendakazi wa watumishi wa umma katika nchi. Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mipango ya kuboresha idara ya NYS eneo la Ruaraka leo, Waziri Kuria alisisitiza umuhimu wa uwajibikaji kwa watumishi wa umma katika kutekeleza majukumu yao.

Kuria alibainisha kuwa wengi wa watumishi wa umma wamekuwa wakijitenga na vikao vya uwajibikaji ambavyo vina jukumu la kutoa taarifa za utendakazi wao. Aliongeza kuwa ni jukumu lao moja kwa moja kwa wananchi na sio kwa viongozi wengine. Aliahidi kuchukua hatua za kuwashurutisha watumishi wa umma kuwajibika kwa wananchi na kuimarisha mifumo ya uwajibikaji katika serikali.

Kauli hii inalenga kuleta mabadiliko katika wizara yake na kuhakikisha kuwa watumishi wote katika nyadhifa za kuwatumikia wakenya wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi na uwazi. Kauli ya waziri Kuria imejiri majuma kadhaa baada ya waziri Kuria kuchukua hatamu za uongozi katika wizara hii baada ya kuhamishwa kutoka wizara ya biashara.

October 25, 2023