AFisa wa zamani wa Magereza akamatwa Transmara

Maafisa wa polisi katika eneo la TransMara, Kaunti ya Narok, wamefanikiwa kumkamata afisa mmoja wa zamani wa idara ya magereza, anayetuhumiwa kuhusika katika njama ya mauaji ya maafisa wawili wa idara hiyo kufuatia mzozo wa kifedha.

Makachero wa idara ya DCI walifanikiwa kumtia nguvuni mshukiwa huyo, ambaye anajulikana kwa jina la Pius Lemiso Ndiwa, katika msitu wa eneo la Maasai Mara mwendo wa saa tano usiku wa Jumanne baada ya kumwinda kwa muda.

Wiki iliyopita, maafisa wawili wa magereza, Inspekta Patrick Mukunyi Kuya na Daniel Nairimo, waliuwawa kinyama baada ya kusafiri katika eneo la TransMara kwa nia ya kutafuta suluhu kuhusu deni ambalo Ndiwa alikuwa anadaiwa na Sacco. Wawili hao walipokelewa kwa mapokezi yasiyofaa na kuvamiwa na watoto wa mshukiwa huyo kwa kutumia mishale na panga hadi kufariki. Inaelezwa kwmaba mshukiwa alikuwa amewaeleza wanawe kwamba kuna wageni watakaowatembelea ni maadui.

Kwa sasa, mshukiwa huyo anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Kilgoris. Uchunguzi zaidi unaendelea kuhusiana na tukio hili la kuhuzunisha.

March 20, 2024