Kenyatta

Usimamizi wa Chuo Kikuu cha Kenyatta umetangaza kusitisha shughuli za masomo katika chuo hicho kwa muda wa siku tatu, kufuatia ajali ya barabarani iliyosababisha vifo vya wanafunzi 11 jana jioni katika eneo la Voi.

Notisi iliyochapishwa pia imeeleza kwamba mipango ya kuhamisha miili ya hadi katika makafani ya hospitali ya chuo inaendelea.

Gavana wa Kaunti ya Taita Taveta, Andrew Mwadime, amethibitisha kwamba serikali ya kaunti hiyo itagharamia ada za matibabu za wanafunzi walioathirika katika ajali hiyo.

Kenyatta University
Picha ya tovuti ya chuo kikuu cha Kenyatta inayotangaza kusitishwa kwa masomo chuoni humo kwa siku 3.

 

Wakati huo huo, Waziri wa Uchukuzi, Kipchumba Murkomen, ametoa tangazo kuhusu hatua za serikali katika kukabiliana na ajali za barabarani. Waziri Murkomen amefafanua kwamba Wizara ya Uchukuzi, kwa kushirikiana na Wizara ya Usalama wa Ndani, zitawarejesha maafisa wa NTSA, ili kuboresha usalama barabarani.

Aidha, ametoa maelekezo ya kufanyika kwa msako wa kitaifa kwa madereva ambao hawazingatii kanuni za trafiki. Murkomen ameagiza kuwafanyiwa mitihani maderava wa uchukuzi wa umma wanaotaka leseni. Pia wananchi wanaotaka kupata leseni watalazimika kufanyiwa vipimo vya kiafya.

 

Msemaji wa Serikali Isaac Mwaura pia ametoa taarifa akiahidi ushirikiano na Chuo Kikuu cha Kenyatta kuhakikisha waathiriwa wanapata matibabu stahiki.

March 19, 2024