Askofu wa Jimbo Katoliki la Ngong, John Oballa Owaa, ametoa wito kwa wanafunzi kuimarisha maisha yao ya sala kama njia ya kukabiliana na changamoto. Askofu alitoa wito huu wakati wa homilia yake kwenye misa ya kusherehekea miaka 60 tangu kuanzishwa kwa Shule ya Wasichana ya St. Mary’s mjini Narok siku ya Ijumaa.

Katika mahubiri yake, Askofu Oballa aliwahimiza wanafunzi kujifunza kutoka kwa Bikira Maria na kutafuta maombezi yake katika kukabiliana na changamoto za maisha. Pia alisisitiza umuhimu wa kuishi maisha yanayompendeza Mungu na kuwataka wazazi kuwafundisha watoto wao kusali bila kuchoka.

Hafla hiyo iliyofanyika siku ya Kumbukumbu ya Bikira Maria Mama wa Mateso, pia ilishuhudia Askofu Oballa akiitabaruku Shule ya St. Mary’s chini ya uangalizi wa Mama Bikira Maria. Huku akizindua Kihekalu cha Mama Maria (Marian Grotto), ambacho kitatoa nafasi kwa wanafunzi, walimu, na wageni kusali wakati wowote. Wakati huo huo, watahiniwa 188 wa darasa la nane na wengine 115 wa Gredi ya sita wanaotarajia kufanya mitihani ya kitaifa ya KCPE na KPSEA mtawalia mwishoni mwa muhula huu, walipata baraka kabla ya mtihani huo.

Mbali na kuhimiza sala na maombezi, Askofu pia alitoa wito wa kuchukua hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kusisitiza umuhimu wa kuyalinda mazingira, yeye mwenyewe akitoa mfano wa kuigwa kwa kupanda mti shuleni kama ishara ya kuunga mkono juhudi za kulinda mazingira.

Mapadre waliokuwepo kwenye misa hiyo walielezea wasiwasi wao juu ya ongezeko la uraibu wa mihadarati, haswa miongoni mwa vijana, na kuwahimiza wanafunzi kuwa waangalifu na kuepuka vitendo vinavyoweza kuwaingiza katika mambo ya kuwapotosha.

 

Share the love
September 15, 2023