Mahakama ya upeo nchini imetoa uamuzi kuhusu uwezo wa maseneta kuwapiga msasa magavana juu ya ukusanyaji wao wa ushuru katika kaunti na vilevile matumizi yao ya fedha wanazokusanya na wanazopokea kutoka katika serikali kuu. Maseneta sasa wana mamlaka ya kuwaita magavana wa kaunti mbalimbali humu nchini katika vikao vyake, ili kujibu maswali au kutoa maelezo zaidi yanayohitajika kutoka kwao.

Mahakama hiyo ya majaji saba chini ya Uongozi wa jaji mkuu nchini Bi. Martha koome imebainisha kuwa kamati ya bunge la seneti inayohusika na kuangazia matumizi ya fedha, ina mamlaka ya kuangazia sio tu mapato na matumizi ya serikali ya kitaifa, bali pia mapato na matumizi ya fedha katika serikali za kaunti. Mahakama hiyo pia imeshikilia msimamo kuwa Mabunge ya Kaunti yana jukumu la kwanza la uangalizi wa mapato ya Serikali ya Kaunti, yawe yanatolewa na serikali ya kitaifa au yanayozalishwa katika kaunti husika. Awali baraza la magavana lilieleza wasiwasi wao kuhusiana na uwezo wa bunge la seneti kutadhmini matumizi yake, baraza hilo likisema kuwa kuwa kamati ya seneti inahusika tu kwa mapato ya kitaifa na sio mapato ya kaunti.

 

Bunge la Seneti, likiongozwa na spika Amason Kingi na naibu wake Murungi Kathuri pia limepewa jukumu la kufuatilia pesa za umma na mienendo ya magavana ili kuhakikisha pesa za walipa ushuru zinatumika kwa njia inayofaa. Kando na mgao wa mapato na matumizi, magavana pia wanatarajiwa kutoa majibu kwa Seneti kwa maswali yote yatakayoibuliwa kuhusu uongozi katika serikali za kaunti. Mahakama aidha iliweka bayana kuwa hakuna chochote kitakacho mzuia gavana kwenda na kikosi chake cha kiufundi au maafisa wengine wa serikali ya kaunti mbele ya kamati ya seneti.

 

October 7, 2022