Mbunge wa Suba Kusini Caroli Omondi ametoa wito wa kufanyika mabadiliko katika chama cha ODM na pia katika muungano wa Azimio la Umoja, hasa kwa viongozi wanaowakilisha muungano huo bungeni, akisema kuwa baadhi ya viongozi wanaohudumu katika nyadhifa mbalimbali hawajaafikia viwango vinavyohitajika.

Akizungumza katika kaunti ndogo ya Uriri alikoandamana na Waziri wa Teknolokjia nchini Eliud Owalo kutwa ya leo, Omondi ameahidi kushinikiza mabadiliko katika wadhifa ya Mnadhimu wa Wachache ambayo kwa sasa inashikiliwa na Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed.

Mbunge huyo ametaja uongozi wa Junet kama uliosababisha chama hicho kupoteza mengi katika bunge hilo, akisema mabadiliko yatahitajika ili kuimarisha chama cha ODM.

Aidha ametetea uongozi wa serikali ya Kenya Kwanza, akisema imeonyesha ishara za kuwa tayari kuleta mabadiliko katika eneo la Nyanza.

December 17, 2022