Ghana - Kenya

Serikali ya taifa la Ghana imeahidi kuunga mkono azma ya Kinara wa chama cha ODM Raila Odinga, ya kuwania wadhifa wa mwenyekiti wa Muungano wa Umoja wa Afrika (AU).

Rais William Ruto, ambaye yupo katika ziara rasmi nchini Ghana, aliweka wazi taarifa hii, akisema kwamba mwenyeji wake, Rais Nana Akufo-Addo, ameunga mkono pendekezo la Kenya katika kugombea uenyekiti wa muungano huo. Rais Ruto ameeleza kwamba Kenya inalenga kuimarisha umoja wa mataifa ya bara la Afrika na kusaidia bara hilo kufikia malengo yake kulingana na ruwaza ya mwaka wa 2063.

YouTube player

Wakati wa ziara hiyo, Rais Ruto alipokea makaribisho ya heshima na kukagua gwaride la heshima. Baadaye, yeye pamoja na mwenyeji wake walishuhudia utiaji saini wa mikataba saba ya makubaliano kati ya Kenya na Ghana. Mkuu wa Baraza la Mawaziri Musalia Mudavadi na waziri wa Ulinzi Aden Duale, ni baadhi ya waliowakilisha Kenya katika hafla hiyo.

Rais William Ruto alisema kwamba mikataba hiyo, ambayo ilijumuisha makubaliano katika maeneo ya sayansi na teknolojia, utalii, elimu, uongozi, na ulinzi, inalenga kukuza biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili.

April 3, 2024