Ajali - Salama Area

Watu kumi wamepoteza maisha yao huku wengine kumi na wawili wakijeruhiwa vibaya katika ajali mbaya ya barabarani iliyohusisha magari kadhaa, ikiwemo matatau na Trella, katika eneo la Salama kwenye barabara kuu ya Nairobi – Mombasa.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa asasi za usalama, ajali hiyo ilitokea baada ya Trella iliyokuwa ikielekea Mombasa kugongana ana kwa ana na matatu iliyokuwa ikielekea Nairobi, kabla ya kugonga magari mengine yaliyokuwa barabarani.

Shughuli za uokoaji zilikumbwa na changamoto kubwa kutokana na mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha katika eneo hilo. Jumla ya magari matano yalihusika katika ajali hiyo iliyotokea mwendo wa saa mbili unusu usiku wa Jumatatu 01 Aprili 2024.

SOMA PIA: Watu 1,026 waaga dunia kufuatia ajali za barabarani mwaka huu

Visa vya Ajali za barabarani vimeongezeka maradufu katika miezi ya kwanza tatu ya mwaka huu, jambo lilimlazimu waziri wa uchukuzi Kipchumba Murkomen kutangaza maagizo mapya ya kukabiliana na visa hivi. Baadhi ya maagizo haya yalijumuisha kurejeshwa barabarani kwa maafisa wa NTSA, kufanyiwa vipimo vya kiafya kwa madereva wa uchukuzi wa umma sawa na mtihani kwa madereva wote kabla ya kupokea leseni.

April 2, 2024