Waziri wa kilimo nchini Mithika Linturi amesema kuwa sajili ya wakulima itakayoundwa baada ya kuwasajili wakulima katika shughuli za kupokea huduma muhimu za serikali kama vile mbegu na mbolea, itawekwa salama.

Waziri Linturi amesema kuwa sajili hii itakapoundwa, itasaidia katika kutekeleza mpango wa serikali wa kuhakikisha taifa linapata chakula cha kutosha kupitia mfumo wa E voucher.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa shughuli za mafunzo ya manaibu kamishena kutoka maeneo yote ya taifa jijini Nairobi, Waziri Linturi amesema kwamba zoezi la usajili lilioanza litaendeshwa kwa mujibu wa sheria na litasaidia serikali na wakulima kutekeleza majukumu yao kwa urahisi. Sajili hii pia inatarajiwa kuisaidia serikali kufahamu mahitaji mbalimbali ya wakulima na kuwawezesha kupokea suluhu la upesi.

Kwa upande wake, katibu mkuu katika wizara ya usalama wandani Raymond Omollo, amesema kuwa shughuli ya usajili itatekelezwa bila malipo na kwa hiari kwa wakulima wanaotaka kufaidi na huduma zinazotolewa na serikali.

Kikao cha mafunzo ya manaibu kamishena kimewaleta Pamoja maafisa 141 pamoja na mawaziri 47 kutoka kaunti zote nchini, wakataotoa mafunzo ya jinsi ya kutekeleza shughuli hii kwa maafisa wengine katika kiwango cha kaunti na wadi.

January 4, 2023