Naibu wa Rais Rigathi Gachagua ameeleza Imani yake kuwa chama cha UDA kitaibuka kidedea katika msururu wa chaguzi ndogo zinazotarajiwa kuandaliwa Alhamisi ya tarehe 5 mwezi huu.

Kipindi cha kampeni kuelekea kwenye chaguzi hizi kimefungwa rasmi jioni ya leo mwendo wa thenashara, ikiwa ni saa 72 kabla ya kufunguliwa kwa vituo vya uchaguzi. Kupitia chapisho kwenye mitandao yake rasmi, Naibu wa rais amesema ushindi wa chama hicho katika chaguzi hizi utasaidia pakubwa katika kutekeleza ajenda ya maendeleo ya serikali ya Kenya Kwanza.

Chama cha UDA kitawakilishwa na Chege Njuguna na Mohammed Dekow katika chaguzi za ubunge katika maeneo bunge ya Kandara na Garrisa Mjini Mtawalia, Abduljabar Saamiya Mohamed katika wadi ya Shella ( Kaunti ya Lamu) huku aliyekuwa mbunge wa Marakwet Magharibi William Kisang akipeperusha bendera ya chama hicho katika kinyang’anyiro cha useneta wa kaunti ya Elgeiyo Marakwet.

January 3, 2023