Viongozi wa kijamii na kisiasa kutoka eneo la Kerio Valley wakiongozwa na Mbunge wa Tiaty William Kamket, wameandaa kikao na wanajamii katika eneo hilo, kwa nia ya kutafuta suluhu la kudumu la vurugu zinazoshuhudiwa katika eneo hilo.

Akizungumza katika kikao hicho, Kamket amewaomba wanajamii kuendelea kutangamana kwa amani kama walivyofanya katika miaka ya awali na kujiepusha na migogoro isiyo wahusu.

Wito huu unakujia saa chache baada ya Waziri wa usala wa ndani Kithure Kindiki, kutoa onyo kali kwa wahalifu katika eneo hilo, akiahidi kuimarisha asasi za usalama ili kuziwezesha kupambana ipasavyo na majambazi. Kindiki alisema haya alipozuru eneo hilo hapo jana, kudadisi hali ya usalama na kutoa hakikisho lake kwa wananchi.

Waziri huyo aliyeandamana na Waziri wa uchukuzi Kipchumba Murkomen pia aliitembelea familia ya Watoto wawili waliouwawa katika shambulizi la wizi wa mifugo siku ya Jumapili.

January 4, 2023