KUTRRH

Hospitali ya Rufaa, Mafunzo na Utafiti ya Chuo Kikuu cha Kenyatta (KUTRRH) imetangaza hatua ya kuwaajiri madaktari watano wa kigeni ili kuongeza uwezo wa kutoa huduma bora za matibabu kwa wagonjwa.

Hatua hii inakuja wakati ambapo matabibu nchini wanashiriki mgomo, ambao umeingia wiki ya nne sasa. Hospitali hiyo yenye uwezo wa kuwahudumia wagonjwa 650 waliolazwa, imekuwa ikitaabika kutokana na mgomo wa matabibu unaoongozwa na muungano wa KMPDU.

SOMA PIA: Madaktari Kushiriki Maandamano ya Amani Jumanne kushinikiza Utekelezaji wa CBA

Kulingana na Profesa Olive Mugenda, mwenyekiti wa bodi inayosimamia hospitali hiyo, kuajiriwa kwa madaktari hao wa kigeni kuna lengo la kuboresha huduma za afya na kuepusha madhara zaidi kwa wagonjwa, haswa wale wanaohitaji matibabu ya Saratani. Profesa Mugenda amesisitiza kwamba madaktari hawa wapya wataendelea kuhudumu kwenye hospitali hiyo hata baada ya mgomo unaoendelea.

Kuhusu mustakabali wa madaktari wa hospitali hiyo ya KUTRRH walio kwenye mgomo, Prof Mugenda amesema wengi wao wamepokea barua za kuachishwa au kusimamishwa kazi.

April 9, 2024