Maandamano ya Madaktari

Muungano wa Madaktari nchini, KMPDU, umetangaza mipango ya kuandaa maandamano ya amani siku ya Jumanne ijayo, lengo likiwa ni kuendelea kuisukuma serikali kusikiliza kilio chao.

Katibu Mkuu wa KMPDU, Davji Atellah, kupitia barua aliyoituma kwa Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Nairobi, Adamson Bungei, akiiomba ulinzi wakati wa maandamano hayo, ameeleza kuwa lengo la maandamano hayo ni kusaidia kuangazia hali ya sekta ya afya nchini.

Dkt.Atelah amekuwa akishikilia kwamba ni sharti serikali itekeleze Mkataba wa maelewano (CBA) wa mwaka 2017 kabla ya madaktari kurejea kazini. Madaktari wamekuwa katika mgomo tangu tarehe 14 mwezi Machi, na kuwaacha watu wanaohitaji huduma za matibabu wakihangaika kutokana na kukosa huduma.

Wakati hayo yakijiri, Kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka, ameendelea kutoa wito wa kupatikana kwa mwafaka wa haraka kati ya serikali na wahudumu wa afya walio kwenye mgomo, ili kukabiliana na mgomo unaoendelea kwa wiki ya tatu sasa.

SOMA PIA: KMPDU Watoa Ilani ya Mgomo Kulalamika Kuondolewa Kwa Ufadhili Wa NHIF.

Kalonzo amesema kwamba muungano wa Azimio utaendelea kupigania na kutetea haki za wakenya wote, huku akisema kwamba amejitolea hata kuwa mpatanishi kati ya serikali na madaktari ili kuhakikisha upatikanaji wa suluhu.

April 5, 2024