Maseneta wamelazimika kukatiza likizo yao ili kuhudhuria kikao maalum cha kusikiliza mswada wa kumbandua gavana wa Meru Kawira mwangaza,  baada ya wawakilishi wadi wa Meru kumbandua mamlakani gavana huyo kwa madai ya utumizi mbaya wa ofisi na kukiuka sheria za katiba.

Katika kikao kilichong’oa nanga adhuhuri ya leo, masenata wamekubaliana kuandaa kamati maalum, itakayochunguza ukweli katika hoja zakumbandua gavana huyo kama zilivyowasilishwa na spika wa bunge la kaunti ya Meru. Seneta wa Kakamega Bonny Khalwale, seneta wa Uasin Gishu Jackson Mandago, Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna na seneta wa Kiambu Karungo Thangwa ni baadhi na maseneta 11 waliotwikwa jukumu la kuwa katika kamati hiyo, ili kuendeleza uchunguzi wa iwapo malalamishi dhidi ya Gavana mwangaza yamefika kiwango kinachosababisha kubanduliwa kwake.

Katika vikao vya leo vya seneti, kauli mseto zilitolewa kuhusu uamuzi wa bunge la Kaunti ya Meru pamoja na uwezo au jukumu la bunge la seneti katika kumbandua gavana.  Hoja ya kubanduliwa kwa Mwangaza ilipendekezwa kwa mara ya kwanza na mwakilishi wadi wa Abogeta magharibi Dennis Kiogora  tarehe 22 mwezi Novemba.

Aidha magavana kupitia baraza la magavana nchini, walijitokeza hiyo jana kusimama na Mwangaza, wakiwaomba maseneta kujikita katika sheria kabla ya kufanya maamuzi ya kumwondoa mamlakani gavana huyo.

December 20, 2022