Na huku Wakenya wakiendelea kukabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi na ukame ambao umetawala kwa muda sasa kutokana na ukosefu wa mvua, maaskofu wa kanisa katoliki wametoa wito  kwa wakenya kushirikiana na kuonyesha ubinadamu kati yao kwa kutoa chakula na msaada wa aina mbalimbali kwa watu walioathirika.

Akitoa wito huu Askofu mkuu wa jimbo kuu katoliki la Nairobi Philip Anyolo, amesema kwamba hata ingawa serikali iko mbioni kuhakikisha usalama wa chakula kwa Wakenya wote, tatizo la uhaba wa chakula na ukame unaoshuhudiwa unahitaji juhudi za pamoja ili kuokoa maisha. Akizungumza baada ya kuweka wakfu kanisa jipya la Mtakatifu Francis wa Assisi katika Kaunti ya Kiambu, Askofu mkuu Anyolo pia ameorodhesha kaunti za Kitui, marsabit, Garrisa, Lodwar kama kaunti ambazo zimeathirika zaidi, huku sasa wakenya wakiombwa kukumbatia roho ya utu na kusaidiana kutatua tatizo hili.

 

October 10, 2022