Kiongozi wa Taiwan ameionya China kwamba taifa hilo la kisiwa kamwe halitaacha kuzingatia utamaduni wake wa kidemokrasia ambapo ametoa ulinganisho na uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine. Watu milioni 23 wa taifa hilo linalojitawala kidemokrasia, wanaishi chini ya kitisho cha kuvamiwa na China mara kwa mara na vita vya Urusi nchini Ukraine vimezidi kuongeza hofu kwamba Beijing inaweza kujaribu kitu sawa na hicho.

Rais wa Taiwan Tsai Ing-wen katika hotuba yake ya siku ya kitaifa hii leo, amesema hawawezi kupuuza changamoto ambazo zinajitokeza. Beijing imejibu hoja hiyo ya rais wa Taiwan kwa kukitaja chama cha rais Tsai kuwa ndio mzizi wa mvutano baina ya pande hizo mbili. China ilikata uhusiano rasmi na Taiwan mwaka 2016 baada ya uchaguzi uliomuweka mamalakani Tsai, kwa sababu anaichukulia Taiwan kama taifa huru na siyo sehemu ya China.

Rais wa Taiwan Tsai Ing-wen
October 10, 2022