Kaunti ya Mombasa imeorodheshwa kama kaunti ambayo ina visa vingi vya unyakuzi wa ardhi nchini. Haya ni kwa mujibu wa Tume ya maadili na kupambana na Ufisadi nchini EACC.

Hata hivyo tume hiyo imefanikiwa kurejesha Vipande vitatu vya Ardhi vilivyokuwa vimenyakuliwa kutoka kwa umma mwaka wa 1991 katika kaunti hiyo ya Mombasa.

Afisa mkuu Mtendaji wa EACC Twalib Mbarak akiandamana na Gavana wa kaunti ya Mombasa Abdullswamad Nassir na Maafisa wengine walizuru ardhi hizo na kutoa taarifa ya pamoja wakieleza kwamba ardhi hiyo imerejeshwa kwa asasi mbalimbali za serikali zilizokuwa wamiliki halisi.

Bw. Mbarak aidha ameeleza kwamba ardhi hizo zinajumuisha makao ya wafanyakazi wa Serikali katika eneo la Buxtan, Nyali, na Shanzu. Aidha mkurugenzi huyo ametoa onyo kwa wote wanaoishi katika ardhi ya umma kuweka mikakati ya kuondoka kwenye ardhi hiyo akisema tume ya EACC haitachoka kufuatilia ardhi zote za umma.

Kauli yake imeungwa mkono na Gavana wa Mombasa Abdulswamad sheriff Nassir ambaye ameeleza kwamba muda wa wanyakuzi wote wa ardhi ya Umma utakamilika na wote waliojitwalia vipande vya serikali watapatikana.

Share the love
November 21, 2023