BY JOHN MSAFIRI

TUMSIFU YESU KRISTO!

Majilio ni nini?
Majilio ni kipindi cha Dominika nne cha kujiandaa na Sherehe ya Kuzaliwa Bwana wetu Yesu Kristo, yaani NOELI.
Kinawakilisha karne zote za Agano la Kale

Katika mwaka wa liturujia ya Kanisa katoliki la Roma ,
sherehe ya Noeli inaandaliwa na kipindi cha
Majilio ambacho kina mambo mawili:
kinakumbusha Mwana wa Mungu alivyotujilia
mara ya kwanza, na papo hapo kinatuandaa
kumpokea atakapotujilia tena siku ya mwisho . Kwa Maana alisema:
“Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu(Mathayo24:42)

Kufuatana na hayo kina sehemu mbili: hadi
tarehe 16 Desemba kinahusu zaidi kurudi kwa
Bwana; siku nane za mwisho kinatuelekeza
moja kwa moja kuadhimisha kuzaliwa kwake.
Urefu wa Majilio unategemea siku
inayoangukia Noeli, kwa kuwa ni lazima yawe
na Jumapili nne. Hivyo basi yanaanza kwa
Masifu ya Jioni ya kwanza ya Jumapili
inayoangukia tarehe 30 Novemba au tarehe ya
jirani zaidi; yanakwisha kabla ya Masifu ya
Jioni ya kwanza ya Noeli.
Kwa jumla ni kipindi cha toba: rangi yenyewe
ni zambarau; haziruhusiwi sherehe za fahari;
ala za muziki na maua vinaweza kutumika
kwa kiasi tu. Masharti hayo yanalegezwa
katika Jumapili ya tatu kwa sababu ya furaha
ya kuona tunakaribia sherehe yenyewe.
Katika kipindi hicho tunaadhimisha tumaini la
Israeli lililotimizwa Yesu alipokuja katika
unyenyekevu wa umbile letu; pia tunangojea
arudi kwa utukufu. Kama alivyotekeleza ahadi
mara ya kwanza, atazitekeleza pia mara ya
pili, ingawa kwake miaka elfu ni kama siku
moja tu.(Zaburi.90) Kati ya majilio hayo mawili, Bwana
anatujilia mfululizo kifumbo katika sakramenti
(hasa ekaristi ) na katika maisha ya kila siku
kwa njia ya matukio na watu (hasa maskini )

Basi tunapaswa kuwa tayari daima kumpokea
ili siku ya mwisho tukamlaki, naye
atukaribishe kwenye uzima wa milele. Pia
tunapaswa kumuomba aje kutukomboa, yeye
aliye tumaini letu.

Katika safari ya Majilio watu watatu
wanatuongoza tukutane na Yesu:

1. Isaya
Nabii wa tumaini, mwenye kipaji cha kutokeza
matazamio ya binadamu na kumhakikishia
atatimiziwa na Mwokozi

2. Yohane Mbatizaji ,
mwenye kuhimiza toba kwa kuwa tunapaswa
kupindua maisha yetu ili tukutane vema na
Kristo.

3. Maria , bikira aliyekuwa tayari
kumpokea Masiya kwa upendo na kushirikiana
naye katika kutimiza mpango wa wokovu .
Tukiwafuata hao watatu tunaweza kujipatia
maadili yale yanayotuandaa kumpokea
Mwokozi anapotujilia: ndiyo matunda maalumu
tunayotarajiwa kuyachuma wakati wa Majilio:

1. Kukesha katika imani, sala na kutambua
ishara za Bwana kutujilia katika nafasi yoyote
ya maisha na mwishoni mwa nyakati.

2. Kuongoka kwa kufuata njia nyofu .

3. Kushuhudia furaha inayoletwa na Yesu kwa
kuwa na upole na uvumilivu kwa wenzetu, kwa
tumaini la kuwa bidii zetu zinawahisha ufalme
wa Mungu wenye heri isiyo na mwisho.

4. Kutunza unyenyekevu kwa kufuata mifano ya
maskini wa Injili ambao ndio waliompokea
Mkombozi .

TUMSIFU YESU KRISTO!👏🏾

November 24, 2022