Makamishna wa IEBC

Kamati ya sheria katika bunge la kitaifa imeanza vikao vya kusikiliza malalamishi yaliyowasilishwa dhidi ya makamishna wanne wa IEBC waliojitenga na matokeo ya uchaguzi mnamo agosti mwaka huu.

Wanne hao ni pamoja na naibu mwenyekiti wa tume hiyo Juliana Cherera, Irene Masit, Justus Nyang’aya na Francis Wanderi.

Chama cha Republican, Dennis Nthumbi, Geoffrey Langat, na Owuor Steve Gerry ambao ni walalamishi waliomba kuondolewa kwa makamishna hao kwa misingi ya utovu wa nidhamu, utumizi mbaya wa ofisi, ukiukaji wa Katiba, na kuegemea upande mmoja kwenye kinyang’anyiro cha urais.

Wakizungumza wakati wa kikao hicho, mawakili wa makamishna hao, wameitaka kamati hiyo kutoshinikizwa na mirengo ya kisiasa wanaposikiliza na hata kutoa uamuzi wa kesi hiyo.

Wakati huohuo baadhi ya wanachama wa kamati hiyo walidinda kuhudhuria kikao cha leo hadi mwisho wakidai kuwa mchakato wa kusikilizwa kwa kesi hiyo haukuwa wa huru na haki. Wakiongozwa na kinara wa wachache bungeni Junet Mohammed, wanachama hao wamedokeza kuwa kuna baadhi ya masuala muhimu ambayo yanapuuzwa na mwenyekiti wa kamati hiyo.

Hali kadhalika Kiongozi wa Azimio la Umoja Raila Odinga amewataka makamishna hao wanne  kususia wito wa kufika mbele ya Kamati hiyo ya sheria .Kulingana na Bw Odinga, matatizo ya sasa yanayowakabili wanne hao ni sehemu ya mpango wa utawala wa sasa kushawishi uchaguzi wa 2027.

Odinga ameongeza kuwa hakuna kamishna aliyepatikana na makosa yoyote ya uchaguzi wakati wa kusikilizwa kwa ombi la Azimio. Aidha ameeleza kuwa utawala wa UDA umekuwa kwenye njia ya kulipiza kisasi tangu kambi yake ilipokubali matokeo ya uchaguzi, ikilenga taasisi na watu ambao hawakuwaunga mkono.

Kwa upande wake kinara wa Narc Kenya Martha Karua amesema kuwa rais Ruto anakiuka sheria kwa kutobuni jopo litakalowateua makamishna wa IEBC ikizingatiwa kwamba mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati pamoja na makamishna wengine wawili wanatarajiwa kustaafu mwaka ujao.

November 24, 2022