Mahakama ya Ajira na leba imetupilia mbali kesi ya kupinga uteuzi wa makatibu waratibu wa wizara mbalimbali.

Ombi hilo liliwasilishwa na Chama cha Wanasheria nchini LSK, kwa misingi ya kutoshirikishwa ipasavyo kwa umma na Tume ya Utumishi wa Umma PSC na kwamba kuwepo kwake kungesababisha matatizo ya kifedha nchini.

Jaji Monica Mbaru aliamua kwamba uamuzi wa PSC kuunda nafasi hiyo ulikuwa halali na kwamba serikali inaweza kuendelea na uteuzi huo.

Mnamo Oktoba, mahakama ilisimamisha uteuzi wa makatibu hao ikisubiri kusikilizwa na kuamuliwa kwa kesi hiyo.

Aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta alizindua nyadhifa za makatibu waratibu mwaka wa 2018, katika hatua ambayo ililenga kuimarisha utendakazi wa Mawaziri.

Wakosoaji hata hivyo wamesema uundwaji wa nafasi hizo unapania kuwatuza watu wanaoegemea upande wa serikali kwa gharama ya walipa kodi.

February 16, 2023