Imram Khan

Mahakama nchini Pakistan imeagiza aliyekuwa waziri mkuu wa zamani Imran Khan kuachiwa kwa dhamana kwa wiki mbili, baada ya kukamatwa kwa madai ya ufisadi, hatua iliyoibua maandamano na ghasia kote nchini humo.

Wafuasi wa chama cha Imran Khan cha Tehreek-E-Insaf waliokuwa nje ya jengo la mahakama walishangilia uamuzi huo na kusema wana imani kwamba maamuzi kama hayo yatalipeleka taifa hilo kwenye mazingira mazuri. Mahakama Kuu ya Islamabad imemuachia Khan kwa dhamana kwa wiki mbili, na kuiagiza taasisi ya kupambana na ufisadi kutomkamata Khan katika kipindi hicho, hii ikiwa ni kulingana na wakili wake Faisal Chaudhry, alipozungumza na shirika la habari la Reuters.

Baada ya agizo hilo la mahakama kutangazwa, waziri wa mambo ya ndani Rana Sanaullah alisema tayari ameyaagiza majeshi ya usalama kuheshimu maagizo ya mahakama na kuonya dhidi ya ukiukwaji wa aina yoyote.

Hapo jana mahakama ya juu zaidi iliamua kiongozi huyo kuachiliwa huru, hatua iliyorejesha utulivu, baada ya taifa hilo kushuhudia makabiliano kati ya wafuasi wa Imran Khan na vikosi vya usalama tangu kiongozi huyo alipokamatwa kwa madai ya ufisadi.

May 12, 2023