Mashambulizi ya makombora katika miji ya Ukraine ukiwemo mji mkuu wa Kyiv, yamesababisha vifo vya watu kadhaa na wengine kujeruhiwa leo Jumatatu, ikiwa ni siku moja baada ya Moscow kuishutumu Kyiv kwa mlipuko uliotokea kwenye daraja linalounganisha Crimea na Urusi.

Kyrylo Tymoshenko, Naibu mkuu wa ofisi ya rais, ametoa wito kwa wakaazi katika miji ambayo imekumbwa na mashambulizi kusalia majumbani na kuongeza kwamba Ukraine ipo chini ya mashambulizi ya makombora. Meya wa mji wa Kyiv Vitali Klitschko amethibitisha kutokea kwa mashambulizi hayo alioyataja kufanywa na Urusi.

Video zilizowekwa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha moshi mweusi ukitanda angani kwenye maeneo kadhaa ya jijini hilo. Rais Volodymyr Zelensky ameituhumu Urusi akisema azma ya Moscow ni kuifuta Ukraine kwenye ramani ya dunia.

October 10, 2022