Mazungumzo yanayolenga kuleta amani mashariki mwa DRC yamefanyika jijini Nairobi ambapo viongozi mbalimbali walihudhuria mazungumzo hayo ili kutafuta suluhu ya kudumu.

Viongozi kutoka jumuiya ya kikanda, Jumuiya ya Afrika Mashariki wanajaribu kuharakisha juhudi zinazoendelea za kikanda ili kufikia amani na usalama endelevu mashariki mwa DRC. Mkutano huo unajiri siku chache baada ya viongozi wa kanda kukubaliana juu ya kusitisha mapigano kufuatia mazungumzo nchini Angola.

Akizungumza wakati wa mkutano huo,msimamizi wa mazungumzo hayo na ambaye pia alikuwa Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amesema kuwa juhudi zaidi zinapaswa kuwekwa katika kuleta amani na utulivu Mashariki mwa DRC.

Aidha Kundi la M23 ambalo limekuwa likipigana na jeshi halitakuwa sehemu ya mazungumzo hayo ikizingatiwa kwamba Serikali ya Congo imekataa kushirikiana na M23 hadi wasimamishe mashambulizi yao na kuondoka katika maeneo ambayo wameyateka katika miezi ya hivi karibuni.

November 28, 2022