BY ISAYA BURUGU 31ST AUG 2023-Mfanyabiashara Nancy Kigunzu, maarufu kwa jina la ‘Mathe wa Ngara’ mitaani, amenyimwa dhamana katika kesi ya kusafirisha dawa za kulevya.Mahakama ilisema katika uamuzi wake kuhusu ombi la dhamana kwamba mfanyabiashara huyo anaweza toroka  iwapo atapewa dhamana kutokana na kujihusisha na ulanguzi wa dawa za kulevya.

Hakimu Njeri Thuku alisema kuwa kumpa dhamana hakukuwa kwa manufaa ya haki.Mfanyabiashara huyo na mshtakiwa wa tatu, Eugine Jumbo, ambaye pia alinyimwa dhamana, wataendelea kuzuiliwa hadi kesi ya ulanguzi wa dawa za kulevya itakaposikilizwa na kuamuliwa.

Wakati huo huo, mshtakiwa mwenzake, Teresia Wanjiru, amepewa dhamana ya Ksh. 50,000 pesa taslimu. Hata hivyo, atahitajika kutoa taarifa za mawasiliano za watu wawili, mmoja ambaye ni ndugu wa damu, na kufika mbele ya mahakama za sheria za JKIA ndani ya siku saba ili kuwasilisha ripoti ya kijamii.

‘Mathe Wa Ngara’ amezuiliwa tangu kukamatwa kwake mnamo Agosti 21 kuhusiana na uvamizi wa dawa za kulevya eneo la Ngara Nairobi, ambapo Ksh.13.4 milioni pesa taslimu pia zilinaswa.

 

 

August 31, 2023