JKIA

Waziri wa Uchukuzi nchini, Kipchumba Murkomen, amechukua hatua kali kufuatia matatizo yaliyotokea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kutokana na hitilafu za umeme katika maeneo kadhaa ya taifa. Matatizo hayo yalisababisha usumbufu mkubwa kwa abiria na shughuli za uchukuzi wa ndege.

Waziri Murkomen amemteua Bw. Henry Ogoye kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (KAA), kikaimu, akichukua nafasi ya Bw. Alex Gitari. Uteuzi huo umefuatia kikao cha dharura kilichoandaliwa na Waziri huyo na maafisa wengine wa mamlaka ya usafiri wa ndege asubuhi ya leo. Waziri Murkomen ametoa ahadi ya kuhakikisha kuwa tatizo lililosababishwa na matatizo ya umeme katika uwanja huo halitajirudia.

Katika mabadiliko mengine yaliyofanywa katika mamlaka hiyo, Bw. Fred Odawo, ambaye alikuwa Msimamizi wa Huduma za Uhandisi, amefutwa kazi na nafasi yake imechukuliwa na Mhandisi Samuel Mwochache kikaimu.

Bw. Abel Gogo, ambaye alikuwa Meneja wa Uwanja wa Ndege wa JKIA, naye amehamishiwa hadi katika Uwanja wa Ndege wa Mombasa. Bw. Peter Wafula amepelekwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kisumu, huku naye Bi. Selina Gor akihamishiwa na kupelekwa katika Uwanja wa Ndege wa JKIA.

Hatua hizi zinachukuliwa kwa lengo la kuboresha usimamizi na utendaji katika mamlaka ya usafiri wa ndege nchini na kuhakikisha usalama na ufanisi katika huduma za usafiri wa anga. Waziri Murkomen alitoa hakikisho kwa wananchi kwamba matatizo ya aina hii hayatashuhudiwa tena katika viwanja vya ndege nchini.

https://twitter.com/kipmurkomen/status/1695428403065762255?s=20

 

August 26, 2023