Gaza

Umoja wa Mataifa umesema leo kuwa msaada usio na kikomo unahitajika Gaza ikiwa ni baada ya wiki tatu za mashambulizi ya Israel ya kujibu uvamizi uliofanywa na Hamas kusini mwa Israel mnamo Oktoba 7.

Mashambulizi hayo yaliyoanza mapema mwezi huu, yamechochea mgogoro wa kiutu katika ukanda huo unaozingirwa wa Kipalestina. Kamishna mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi wa Kipalestina – UNRWA, Philippe Lazzarini, amesema msaada wa kutosha unahitajika katika Ukanda wa Gaza, huku akieleza kwamba msaada unaoingia katika eneo hilo kwa sasa ni kama makombo.

Lazzarini pia amethibitisha kuwa wafanyakazi 57 wa shirika hilo wameuawa katika vita hivyo. Vita kati ya Israel na vuguvugu la Hamas, vinaendelea kusababisha uharibufu kwa maelfu ya wananchi katika eneo la Gaza linaloamikiwa kuwa ngome ya Hamas.

Hadi kufikia sasa idadi ya Wapalestina waliouawa imezidi 7,000, wakati Jeshi la Israel likiendeleza mashambulizi makali ya angani, huku wakiweka mipango ya kufanya uvamizi kamili wa ardhini.

 

 

October 27, 2023