Mamlaka ya Mawasiliano nchini  imetangaza nafasi ya kazi  ya Mkurugenzi Mkuu ambayo awali ilikuwa ikishikiliwa na  Ezra Chiloba ambaye alijiuzulu wiki jana.
Chiloba aliyejiuzulu kutoka wadhifa huo tarehe 18 mwezi huu na kuashiria mwisho wa miaka miwili katika mamlaka hiyo.

Katika notisi katika magazeti ya kila siku, Mamlaka hiyo iliwaalika watu waliohitimu kutuma maombi yao kufikia saa kumi na moja jioni siku ya Ijumaa, Novemba 17.

Kwa mujibu wa notisi hiyo, waombaji wanatakiwa kuwa na Shahada katika mojawapo ya kozi zifuatazo : Mawasiliano, Teknolojia ya Habari, na Sayansi ya Jamii.

Ili kupata nafasi hiyo mgombea anatakiwa pia kuwa na ujuzi katika matumizi ya kompyuta na kutimiza matakwa ya Sura ya Sita ya Katiba kuhusu Uadilifu.

Kwa uzoefu wa kazi, waombaji wanatakiwa kuwa na uzoefu wa kazi usiopungua miaka kumi (10) na angalau miaka mitano (5) katika usimamizi mkuu.

Ujuzi unaohitajika ni pamoja na ujuzi wa kifedha na uwezo wa kuhamasisha na kusimamia rasilimali kwa ufanisi na ujuzi wa teknolojia zinazoibuka na athari zake kwenye sekta.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano ndiye Mtendaji Mkuu na Afisa Masuuli wa Mamlaka anayesimamia shughuli za kila siku, akitoa uongozi wa jumla na ndiye msemaji wa Mamlaka katika masuala yote ya kiutendaji.

DG ana jukumu la kutoa uongozi wa kimkakati, kuweka dira ya wazi ya CA, na kuoanisha shughuli zake na malengo ya kitaifa na kisekta.

Share the love
October 27, 2023