Waziri wa usalama wa ndani Kithure Kindiki ameongeza muda wa kutotoka nje kuanzia jioni hadi alfajiri katika eneo la Chakama Ranch kwa siku 30.

Akizungumza mjini Malindi alikoenda kusimamia kuanza kwa uchunguzi wa miili 125 iliyofukuliwa katika msitu wa Shakahola Kindiki pia aliongeza hatua nyingine zote alizotoa mnamo Aprili 26, 2023.

Hii ina maana kwamba hakutakuwa na mikusanyiko ya watu wote au maandamano katika kipindi hicho cha siku thelathini.

Waziri huyo pia alitangaza kuwa eneo hilo linasalia kuwa eneo la uhalifu na nje ya mipaka kwa kila mtu ambaye hajaidhinishwa.

Wakati hayo yakijiri zoezi la uchunguzi wa miili 125 iliyofukuliwa katika msitu wa Shakahola lilirejelewa hii leo. Miili hiyo iliyopolewa katika awamu ya pili ya zoezi la ufukuaji ambapo hadi sasa jumla ya maiti 241 zimetolewa msituni.

Zoezi hilo la uchunguzi wa maiti linafanyika katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Malindi. Miili hiyo inaaminika kuwa ya waathiriwa wa dhehebu linaloongozwa na mhubiri Paul Mackenzie ambaye anadaiwa kuwalazimisha waumini wake kufunga kula kwa siku kadhaa.

May 25, 2023