Muungano wa Kenya Kwanza umezindua timu ya watu 5 watakaoshiriki mazungumzo ya kutafuta mwafaka kati ya serikali na upinzani.

Kiongozi wa Wengi katika bunge la kitaifa Kimani Ichung’wah ataongoza timu hiyo, ambayo pia itajumuisha Kiongozi wa Wengi katika bunge la Seneti Araon Cheruiyot na Gavana wa Embu Cecily Mbarire. Wajumbe wengine walioteuliwa kwenye mazungumzo hayo ni pamoja na Hassan Omar na Catherine Wambilianga.

Timu ya Kenya Kwanza pia iliorodhesha ajenda tano ambazo wananuia kujadiliana na muungano wa Azimio, ikiwa ni pamoja na kuunda upya IEBC na kutekelezwa kwa sheria ya thuluthi mbili ya jinsia.

Masuala mengine ambayo timu ya Kenya Kwanza inanuia kuzungumzia ni pamoja na kuanzishwa kwa ofisi rasmi ya kiongozi wa upinzani, kuanzishwa kwa Hazina ya Maendeleo ya Maeneo Bunge, na kuzinduliwa kwa afisi ya Mkuu wa Mawaziri.

Aidha muungano huo umedai kuwa hakutakuwa na mjadala wa aina yoyote kuhusu handisheki. Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya ulitaja wanachama watano kwenye ujumbe wake Jumatatu.

Ujumbe huo utaongozwa na Kiongozi wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka na utajumuisha Kiongozi wa Wachache Opiyo Wandayi na Kiongozi wa Chama cha DAP Eugene Wamalwa.

Wengine ni pamoja na Seneta wa Nyamira Okon’go Omogeni na Mbunge wa Malindi Amina Mnyazi. Duru hii mpya ya mazungumzo hayo inajiri siku chache baada ya Rais William Ruto na kiongozi wa upinzani Raila Odinga kufanya mazungumzo ya kwanza kati ya msururu wa mazungumzo yaliyosimamiwa na aliyekuwa Rais wa Nigeria Olusegun Obasanjo.

Rais Ruto, ambaye alithibitisha mkutano huo, alisema kuwa mkutano wa kwanza ulinuiwa kuweka msingi wa mazungumzo hayo.

Share the love
August 2, 2023