Kaunti ya Meru kwa mara nyingine imegonga vichwa vya habari kufuatia mzozo mpya unaonukia baada ya Naibu Gavana wa kaunti hiyo Isaac Mutuma kutoa malalamishi mapya dhidi ya Gavana Kawira Mwangaza.

Mutuma amejitokeza na kudai kuwa Gavana Mwangaza anamtaka ajiuzulu kama naibu gavana. Aliongeza kuwa Mwangaza amekuwa akiwasiliana naye kupitia wawakilishi wake na kumtaka aondoke kwenye nafasi yake na apate malipo ya kuachishwa kazi.

Mzozo huu wa hivi punde ni miongoni mwa mizozo ambayo imekumba kaunti ya Meru tangu uchaguzi mkuu wa Agosti 2022.

Itakumbukwa kwamba gavana Mwangaza ametimuliwa madarakani  mara mbili na Bunge la Kaunti ya Meru, baada tu ya hatima yake kuamuliwa na Seneti ambayo ilimrejesha kazini.

Wawakilishiwadi walikuwa wamemshtumu Mwangaza kwa ufisadi, utumizi mbaya wa ofisi miongoni mwa mengine, madai ambayo Seneti ilitaja kuchochewa kisiasa.

Mwangaza kwa upande wake alidai kuna watu wenye nguvu ambao hawafurahishwi na uongozi wake, na wanafanya kila wawezalo kumfukuza ofisini.

February 28, 2024