Pope Francis amzika Pope Benedict XVI

Kiongozi wa kanisa Katoliki Papa Francis mchana wa leo ameongoza misa ya ibada ya mazishi ya mtangulizi wake Papa Benedict XVI mjini Vatican.

Papa Francis ametoa mahubiri katika Misa hiyo ambayo imehudhuriwa na takriban makadinali 120, maaskofu 400 na Zaidi ya mapadre 4,000 katika uwanja mkubwa wa Kanisa la Mtakafitu Petro, kabla ya mwili wa papa huyo mstaafu kuzikwa katika makaburi ya mapapa chini ya kanisa hilo.

Waumini wapatao 60,000 wamehudhuria misa hiyo wakiwemo wajumbe rasmi kutoka mataifa mbalimbali ulimwenguni. Mataifa mengine pia yamewakilishwa na mabalozi wao mjini Vatican. Papa Benedict, ambaye jina la kuzaliwa ni Joseph Ratzinger, aliaga dunia siku ya Jumamosi iliyopita akiwa na umri wa miaka 95.

Humu nchini, mwakilishi wa papa katika taifa la Kenya na Sudan Kusini Askofu mkuu Hubertus Matheus Maria van Megen, aliongoza ibada ya misa takatifu kumwomboleza Papa Mstaafu Benedict XVI katika kanisa kuu la Holy Family Jijini Nairobi, ambapo amemtaja papa huyo kama kiongozi aliyeipenda kanisa, na aliyekuwa na moyo wa kujiimarisha kwa kujiongezea masomo. Pia alitoa historia fupi ya Maisha ya papa huyo akisifia mahusiano waliokuwa nayo wakati wa uongozi wake.

Misa hiyo ilihudhuriwa na viongozi wengine wa kidni akiwemo Mwadhama kadinali John Njue na maaskofu wakuu akiwemo Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Nairobi Philip Anyolo na wawakilishi kutoka mataifa Jirani, wote wakituma rambirambi zao kwa waumini kote ulimwenguni.

Miongoni mwao pia alikua askofu wa jimbo katoliki la Ngong John Oballa Owaa ambaye aliteuliwa kuwa askofu na Papa Benedict XVI.

SOMA PIA

Maelfu wajitokeza kumuaga Papa Mstaafu Benedict XVI mjini Vatican.
TAANZIA: Papa Mstaafu Benedict XVI ameaga dunia!

Fuatilia Misa ya mazishi ya Papa Benedict XVI HAPA

January 5, 2023