Papa Francis Padre John Njue Njeru Kuwa Msimamizi wa Kitume wa Jeshi la Kenya

Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani, Papa Francis, amemteua Luteni Kanali Padre (Monsignor) Mons. John Njue Njeru kama Msimamizi wa Kitume wa idara ya jeshi nchini Kenya. Taarifa ya uteuzi huu ilitangazwa siku ya Jumanne, Januari 30 na Baraza la Maaskofu wa kikatoliki nchini Kenya (KCCB).

Luteni Kanali Padre Njue amechukua wadhifa huo kutoka kwa mtangulizi wake, Padre (Mons.) Benjamin Kituto Maswili, ambaye amestaafu baada ya kufikisha umri wa miaka 60. Padre (Mons.) Maswili amehudumu kama mchungaji wa kitume katika idara ya jeshi tangu mwaka 2016. Kabla ya uteuzi huu, Padre (Mons.) Njue alikuwa akihudumu katika ofisi ya Msimamizi wa Kitume katika Makao Makuu ya idara ya Ulinzi nchini.

Padre (Mons.) Njue, alizaliwa mwezi Julai 1972, na kutawazwa kuwa Kasisi wa Jimbo Katoliki la Embu mwezi Aprili 2002. Katika kipindi chake cha utumishi, Padre (Mons.) Njue alishikilia nyadhifa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuwa Afisa wa Wafanyakazi na Kasisi katika Makao Makuu ya Jeshi la Wanamaji lenye makao yake eneo la Mtongwe, Mombasa huku pia akishiriki katika Misheni ya kulinda amani nchini Somalia.

Padre (Mons.) Njue anakuwa Msimamizi wa pili wa Kitume wa Kijeshi, ambalo lilianzishwa mnamo Januari 1964 kama vikarieti, kabla ya kupandishwa cheo kuwa kituo cha kitume cha kijeshi mwaka 1981, ili kutoa huduma za kichungaji kwa Wakatoliki wanaohudumu katika idara ya Jeshi la Kenya (KDF) na familia zao.

 

January 31, 2024