Wizara ya Afya imetoa tahadhari ya afya ya umma kuhusu kuenea kwa ugonjwa wa macho wa Conjunctivitis. Huku akihamasisha umma kuhusu mkurupuko huo, Mkurugenzi Mkuu katika wizara ya Afya, Patrick Amoth alisema ugonjwa huo umekithiri katika eneo la Pwani haswa Malindi, Lamu na Mombasa na unaonyesha dalili za macho mekundu.

Aidha alisema ugonjwa huo kwa kawaida huenezwa kwa kugusa macho ya watu walioambukizwa au sehemu zilizoambukizwa kisha kugusa macho ya mtu ila hakuna sababu ya kutisha kwani kwa kawaida hujizuia.Wale wanaopata dalili kali ambazo ni pamoja na uwekundu, kutokwa na uchafu, uvimbe au kutokwa na damu wamehimizwa kutafuta matibabu ya haraka.

Baadhi ya visa vichache vya ugonjwa huo vimeripotiwa katika maeneo mengine ya nchi huku Kaunti za Kisii na Nairobi zikirekodi kisa kimoja na watatu mtawalia.

January 31, 2024