Papa Francis

Kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis, anapeleka ujumbe wake wa “uwepo wa majadiliano” kwa ulimwengu wa kiislamu nchini Bahrain, ambako serikali hiyo inayoongozwa na madhehebu ya wasuni imeandaa mkutano wa kidini unaohimiza utangamano kati ya mataifa ya Mashariki na Magharibi, licha ya kushutumiwa kwa kuwabagua waumini wa madhehebu ya washia walio wengi nchini humo.

Makundi ya kutetea haki za binaadamu na jamaa za wanaharakati wa kishia, waliohukumiwa kifo, wamemtolea mwito Papa Francis kutumia ziara hiyo kuitaka serikali kufuta hukumu ya kifo na ukandamizaji wa kisiasa Bahrain. Papa Francis anafanya ziara ya siku nne na ambayo ni yake ya kwanza kabisa nchini humo. Ziara hiyo pia ni ziara ya kwanza kufanywa na kiongozi wa kanisa Katoliki katika taifa hilo la Bahrain.

Papa Francis anasisitiza kuwa mazungumzo ndiyo njia pekee ya upatikanaji wa amani na kuamini kwamba maelewano ya kidini yanahitajika hasa wakati huu wa vita vya Urusi na Ukraine na migogoro ya kikanda kama ile inayotokea Yemen.

November 3, 2022