Rais William Ruto ameunda Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na jinamizi la Ukame, kamati itakayoongozwa na Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa kampuni ya mawasiliano ya Safaricom Peter Ndegwa.

Kulingana na Notisi ya Gazeti la Serikali iliyochapishwa hii leo, uundaji wa kamati hiyo ulitokana na hitaji la kuanzisha mfumo wa kukusanya rasilimali za ziada ili kushughulikia athari mbaya za ukame. Kamati hiyo inatarajiwa kuangazia maeneo kama vile chakula, maji, mifugo, afya, wanyamapori, nishati, elimu, usalama, misitu, kilimo na unyunyizaji maji.

Kamati hiyo imetwikwa jukumu la kuanzisha Hazina ya Kitaifa ya Kukabiliana na Ukame humu nchini, itakayoongozwa na sekta ya kibinafsi chini ya ufadhili wa Shirika la Msalaba Mwekundu, pamoja na kukusanya rasilimali ili kusaidia mpango wa serikali wa kukabiliana na ukame ili kupunguza athari za ukame ulioenea maeneo tofauti ya taifa.

Kamati hiyo, inayojumuisha wajumbe 13 wakiwemo wakuu wakuu wa makampuni, na itahudumu kwa muda wa mwaka mmoja kutafuta rasilimali ili kuongeza mpango wa serikali wa kukabiliana na ukame katika kupunguza athari za ukame nchini.

Wanachama wengine katika kamati hiyo ni pamoja na James Mwangi (CEO Equity Bank), Nasim Devji (CEO Diamond Trust Bank), Shumaz Savani (CEO ABC Bank), Paul Rushdie Russo (CEO KCB), Rebecca Mbithi (CEO Family Bank), Jane Karuku (Mkurugenzi Mtendaji wa EABL), Joshua Chepkwony (CEO Jamii Telcom) na Crispin Acholla (CEO British American Tobacco )

November 21, 2022