Rais William Ruto amejitolea kutoa pesa kwa wakati kwa serikali za kaunti akidai kuwa hatua hiyo itaharakisha ukuaji wa ugatuzi na kurahisisha utoaji huduma.

Akizungumza wakati wa Mkutano wa 9 wa Kitaifa na Uratibu wa Kaunti unaoendelea kule Naivasha kaunti ya Nakuru,rais amebainisha kuwa vitengo vya utawala vilivyogatuliwa ndivyo viachangia asilimia kubwa ya maendeleo nchini.

Ameahidi kufanya kazi kwa karibu na kaunti na kuongeza ushirikiano haswa katika sekta za kilimo, usalama, afya na makaazi. Aidha rais amewataka viongozi hao kujitahidi kuimarisha maelewano kati yao, kuungana na kushirikiana mara kwa mara.

Naibu rais Rigathi Gachagua kwa upande wake ameeleza kuwa ni lengo la Serikali kuhakikisha ugatuzi unafaulu.

Viongozi wengine ambao wamehudhuria mkutano huo ni pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la Magavana Ann Waiguru, Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula, Spika wa Seneti Amason Kingi, Mwanasheria Mkuu Justin Muturi.

February 10, 2023