Rais William Ruto asaini Sheria mpya

Rais William Ruto, ameendeleza ziara yake katika ukanda wa Nyanza kwa kuongoza kikao cha baraza la mawaziri katika ikulu ya Kisumu asubuhi ya leo.

Rais Ruto, ambaye amekuwa katika ziara ya kikazi katika eneo hilo tangu Ijumaa, anatarajiwa kumaliza ziara yake ya kwa kuzindua miradi kadhaa ya maendeleo hii leo.Kikao hiki cha baraza la mawaziri kimeandaliwa siku chache baada ya mabadiliko ya hivi karibuni katika mpangilio wa serikali, ambapo mawaziri saba walipata kuhamishwa hadi wizara tofauti.

Kabla ya kuanza kwa kikao cha baraza la Mawaziri, rais alitia saini Mswada wa Ubinafsishaji wa 2023 kuwa sheria. Sheria hii sasa itaiwezesha serikali kuendeleza mchakato wa kubinafsisha idara mbalimbali za serikali ambazo zimekuwa zikisajili hasara. Mswada huu uliowasilishwa na Kinara wa wengi katika bung ela kitaifa Kimani Ichung’wa unatarajiwa kuhusisha sekta za kibinafsi zaidi katika maendeleo.

Miongoni mwa miradi ambayo Rais anatarajiwa kuizindua leo ni pamoja na meli ya MV Uhuru II. Meli hii itatumika katika Ziwa Viktoria na itasaidia kuboresha usafiri wa majini na kurahisisha shughuli za biashara na usafirishaji katika eneo hilo.

Adhuhuri ya leo, kiongozi wa taifa ameratibiwa kuzindua ujenzi wa Barabara ya Bondo-Liunda, katika eneo bunge la Bondo.

 

Share the love
October 9, 2023