By Isaya Burugu/DW,Oct 12,2022-Ujerumani imerejea katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, baada ya kuchaguliwa katika Baraza Kuu la umoja huo jana jioni. Nchi nne za Afrika; Sudan, Algeria, Moroko na Afrika Kusini pia zimechaguliwa.

Kura hiyo ya siri ilipigwa kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lenye nchi wanachama 193, kujaza nafasi 14 kwenye Baraza la Haki za Binadamu lenye viti 47. Ujerumani imepita kwa kupata kura 167 katika ya 176 zinazowezekana, ikiwa na maana kuwa itakaa katika baraza hilo kwa miaka mitatu, kuanzia 2023 hadi 2025.

Nchi nyingine zilizofanikiwa kuchaguliwa katika baraza hilo ni Algeria, Bangladesh, Ubelgiji, Chile, Costa Rica na Georgia. Nyingine ni  Kyrgyzstan, Maldives, Moroko, Romania, Afrika Kusini, Sudan na Vietnam.Venezuela, Korea Kusini na Afghanistan pia zilijaribu lakini zilishindwa kupata kura za kutosha kuziunga mkono.

Viti katika baraza hilo husambazwa katika utaratibu unaohakikisha kuwa kanda zote za dunia zinawakilishwa. Makundi ya kutetea haki za binadamu yanaukosoa mtindo huo, kwa hoja kwamba unazinyima nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa chaguo huru la nchi zifaazo, na kuzihakikishia nafasi baadhi ya nchi zenye rekodi mbaya ya haki za binadamu.

October 12, 2022