BY ISAYA BURUGU,4TH ,NOV 2022-Watu watatu wametiwa mbaroni katika kaunti ya Homa Bay kuhusiana na ulanguzi wa Watoto.Kwa mjibu wa taarifa kutoka kwa polisi ni kwamba maafisa wa usalama walipata Habari  kuwa gari moja la kibinafsi lilikuwa linamsafirisha mtoto kutoka Oyugis  kuelekea mjini  Kendu Bay.

Uchunguzi wa awali umefichua kuwa mtoto huyo alikuwa tayari ameuzwa kwa mtandao wa ulanguzi wawatoto kwa shilingi alfu 80 mjini  Keroka kaunti ya Nyamira.

Polisi waliliwekea mtego gari hilo lenye nambari za usajili KCW 901Y na kulinasa ambapo dereva aliwaelekeza polisi  kutoka kituo cha polisi cha Kendu Bay hadi kwa nyumba moja katika Kijiji cha Nyaburi  huko Karachuonyo  ambapo watatu hao miongoni mwao mwanamke wa miaka 62 walikamatwa.

Msako uliendeshwa  katika nyumba hiyo na mvulana wa miaka 2 akapatikana.Kufuatia hali hiyo watatu hao  , Ruth Aoko Awuor, Winny Ginjo na Molly Akinyi wamekamatwa  na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani ambapo watakabiliana na mashtaka ya ulanguzi wa binadamu.

 

 

 

November 4, 2022