EWASO NGIRO

Wafugaji na wakulima wa mifugo katika kaunti ya Narok wameshauriwa dhidi ya kuendelea na hulka ya kuweka alama kwenye ngozi za mifugo yao. Ushauri huu umetolewa na viongozi mbalimbali, wakiwemo katibu katika idara ya mifugo nchini, Jonathan Mwake, na naibu gavana wa kaunti ya Narok, Tamalinye Koech. Viongozi hawa wameeleza kuwa kuweka alama kwenye ngozi imekuwa ikiathiri ubora wa ngozi inayouzwa kwenye viwanda vya ngozi.

Jonathan Mwake, akizungumza na waandishi wa habari alipotembelea kiwanda cha ngozi katika eneo la Ewaso Ngiro Narok, alisema kuwa mazoea ya kuweka alama kwenye ngozi yamekuwa yakipunguza ubora wa ngozi na hivyo kuathiri bei inayopatikana sokoni.

Kwa upande wake, Naibu gavana wa kaunti ya Narok, Tamalinye Koech, aliwataka wafugaji kuwa makini wanapoweka alama kwenye ngozi za mifugo yao ili kuhifadhi thamani ya ngozi hizo, akiwashauri pia kutafuta soko la kuuza ngozi kila wanapowachinja mifugo wao, ili waweze kufaidi pia.

Ngala Oloitiptip, meneja wa Mamlaka ya Maendeleo ya Ewaso Ngiro Kusini (ENSDA), alisema kuwa kwa sasa mamlaka hiyo inanunua ngozi kutoka kwa wafugaji kwa bei nafuu, huku akiwataka wafugaji kuhakikisha ngozi wanazopeleka sokoni zina ubora wa hali ya juu ili kuwahakikishia bei nzuri ya kuwafaidi.

Taarifa yake Antony Mintila | mmintila@radioosotua.co.ke | radioosotua.co.ke

Share the love
August 29, 2023