Watoto wawili kati ya wanne waliopewa sumu na kudungwa kisu na baba yao Jumanne usiku walifariki wakitibiwa katika hospitali ya rufaa ya Homa Bay.

Haya yanajiri baada ya baba yao Ronnie Ochieng’ Nyore kuwadunga kisu watoto hao nyumbani kwao katika eneo la Kochia mashariki kwa madai ya ugomvi wa kinyumbani na mkewe na baadaye kufariki kwa kujitoa uhai.

Odongo na Opiyo, mapacha wenye umri wa miaka mitatu, wanasemekana kufariki Jumatano usiku baada ya kuzidiwa na makali ya sumu, ambayo iliathiri ubongo wao na viungo vingine vya ndani. Opiyo alifariki dunia katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) huku kakake akiaga dunia alipokuwa akipokea matibabu katika wadi ya jumla.

Mama yao ambaye anadai kuwa anahangaika kutafuta riziki, sasa anaomba msaada kwa umma akibainisha kuwa familia ya mumewe imemtenga.

Aidha Daktari Charles Ochola, amethibitisha kuwa watoto wawili waliosalia wako katika hali nzuri.

December 8, 2022