Watu watatu waliuawa baada ya mapigano mapya kuzuka kati ya jamii zinazoishi kwenye mpaka wa Kisumu na Kericho.

Wengine wengi wanauguza majeraha baada ya wavamizi waliokuwa wamejihami kwa silaha kushambulia wanakijiji katika eneo la Kadiang’a Mashariki katika Kaunti Ndogo ya Nyakach.

Kikosi cha Usalama cha Kaunti ya Kisumu wakiongozwa na Kamishna wa Kaunti hiyo Hussein Alassow Hussein wamefanya mkutano katika eneo hilo ili kutuliza mvutano kati ya jamii hizo mbili.

Hussein alisema maafisa wa polisi wametumwa kusaidia kurejesha hali ya utulivu.Kwa upande wake Gavana wa Kaunti ya Kisumu Prof. Anyang Nyong’o alikashifu mashambulizi hayo akisema ni bahati mbaya kupoteza maisha kwa njia hiyo.

Alivitaka vyombo vya usalama kuwakamata haraka wale waliohusika na mashambulizi hayo na kuhakikisha haki inatendeka kwa familia zilizoathirika.

October 4, 2023