Waziri wa usalama wa ndani Kithure Kindiki ameendelea na ziara yake ya kutathmini hali ya usalama katika eneo la kaskazini mwa bonde la ufa ambapo amezuru kaunti ya Laikipia hii leo.

Kindiki amewahimiza wakaazi wa eneo hilo kutohusisha vita dhidi ya ujambazi na misingi ya kisiasa, kabila, utamaduni au dini huku akiwarai viongozi wa kisiasa kutoingilia masuala ya usalama wa taifa.

Waziri huyo pia alisema kuwa vita dhidi ya ujambazi vitaimarishwa ili kukomesha tishio la muda mrefu ambalo limekatisha tamaa amani katika eneo la North Rift. Kando na hayo aliongeza kuwa maafisa wa usalama waliotumwa katika kaunti sita zinazoshuhudia mashambulizi ya mara kwa mara watasalia huko hadi pale wahalifu watakapopokonywa silaha zao zote.

November 2, 2023