Kithure Kindiki

Waziri wa usalama wa ndani Prof Kithure Kindiki ametoa Onyo kali kwa wahalifu wanaowahangaisha wananchi katika maeneo tofauti ya taifa, akisema kuwa serkali imeweka mipango kabambe ya kukabiliana nao ili kuhakikisha kuwa wakenya wanaendelea kutekeleza majukumu yao kwa amani pasi na hofu ya lolote.

Akizungumza katika kikao na waandishi wa habari jijini Nairobi, Waziri Kindiki amesema kuwa wahalifu na wezi wa mifugo katika maeneo ya kaskazini mashariki pia hawatasazwa kwani maeneo hayo pia yanahitaji kushuhudia maendeleo kama maeneo mengine ya taifa.Katika taarifa yake, Kindiki ameonekana kuwapa amri maafisa wa polisi katika jiji la Nairobi kuwakabili ipasavyo genge la wahalifu lililojitokeza na kuanza kuwatishia maisha wananchi kwa kuwadunga visu.

Kauli sawia pia imetolewa na Inspekta Jenerali wa polisi nchini Bw. Japheth Koome ambaye amesema kuwa sheria za taifa zimeweka bayana kuwa uhalifu wa wizi wa mabavu una adhabu kali na hivyo kuwaonya wanaotekeleza hulka hii kuwa chuma chao ki Motoni.

November 14, 2022