Bunge la Taifa limeidhinisha rasmi uteuzi wa makamishna wapya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC, katika kikao cha Jumatano 04.o6.2025. Ripoti ya Kamati ya Sheria bungeni (yaani JLAC) iliwasilishwa bungeni siku ya Jumanne kwa mjadala na hatimaye kuungwa mkono na wabunge kwa kauli moja kwenye vikao vya Jumatano.
Kwa sasa, makamishna hao wanasubiri hatua ya kuapishwa kabla ya kuanza rasmi kazi zao katika tume hiyo yenye majukumu ya muhimu kwa taifa. Hata hivyo, utekelezaji wa hatua hizo unakumbwa na kizingiti cha kisheria, kufuatia kesi iliyoko mahakamani inayopinga baadhi ya vipengele vya uteuzi huo.
Mahakama tayari imetoa amri ya kusitisha kuchapishwa kwa majina ya makamishna hao kwenye gazeti rasmi la serikali, pamoja na kuzuia kuapishwa kwao, hadi pale uamuzi kamili wa kesi hiyo utakapotolewa.