usajili wa wapiga kura IEBC

    Tume ya Uchaguzi na Uratibu wa Mipaka nchini (IEBC) imetangaza kuwa imewasajili wapiga kura wapya 531,185 kati ya tarehe 3 Aprili na jioni ya Ijumaa, tarehe 10 Aprili mwaka huu.Katika taarifa yake, IEBC imesema jumla ya wapiga kura wapya sasa imefikia 875,501. Pia, wapiga kura 49,502 wamehamisha vituo vyao vya kupigia kura.

    Kaunti ya Nairobi inaongoza kwa usajili ikiwa na wapiga kura wapya 96,897. Kaunti nyingine zilizoongoza ni Kiambu (46,265), Kakamega (40,110), Nakuru (32,559) na Machakos (30,686).Kwa upande mwingine, kaunti zilizo na idadi ndogo ni Nyamira (8,146), Nyandarua (7,906), Mandera (7,337), Isiolo (5,379) na Lamu (4,810) .

    Katika Kaunti ya Narok, wapiga kura wapya waliosajiliwa wamefikia 18,937 hadi sasa.

    Wakati huo huo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa IEBC, Moses Sunkuli, amesema hakuna mtu atakayezuiwa kujisajili iwapo anakidhi vigezo. Ameongeza kuwa zoezi la usajili linaendelea. Sunkuli amewahimiza Wakenya ambao hawajajisajili kutumia fursa iliyopo sasa. Amesema kila mwananchi ana haki ya kushiriki katika uchaguzi mkuu.

    Akizungumza baada ya kikao cha Kamati ya Bunge kuhusu Katiba na Utekelezaji, Sunkuli alisema zoezi la usajili limechelewa kufanyika. Wanachama wa tume hiyo pia wametaka juhudi zaidi zifanywe mashinani. Wamesisitiza umuhimu wa kuwafikia watu wanaoishi na ulemavu kote nchini.

    April 11, 2026