Tume ya huduma za waalimu nchini (TSC) imetangaza kuwa waalimu wapatao 14,460 wameajiriwa na kutumwa katika shule mbalimbali kote nchini, kama mojawapo ya njia za kukabiliana na uhaba wa waalimu. Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa TSC Dkt. Nancy Macharia alitoa tangazo hilo mchana wa leo wakati wa maadhimisho ya siku ya waalimu duniani katika chuo cha Serikali jijini Nairobi. Dkt. Macharia ameweka wazi kuwa waalimu hao waliajiriwa katika zoezi la uajiri lililotekelezwa katika maeneo tofauti ya taifa mwezi septemba 2022. 

Zaidi ya hayo amesisitiza kuwa hatua hiyo itasaidia zaidi katika kukabiliana na changamoto ambazo zimetokana na uhaba wa walimu kufuatia kuazishwa kwa shughuli za mpito wa asilimia 100 ya wanafunzi kutoka shule za msingi hadi shule za upili. Taarifa yake inajiri katika kipindi ambacho taifa pia linajiandaa kwa mitihani ya kitaifa katika kipindi cha miezi miwili ijayo, kwa watahiniwa wa kidato cha nne, darasa la nane na pia Gredi ya sita.

Dkt. Macharia aidha amempongeza Rais William Ruto kwa kujitolea kuimarisha sekta ya elimu nchini, na hasa kwa uamuzi wake wa kuunda jopokazi litakalosaidia katika kuangazia ufaafu na jinsi mfumo mpya wa elimu wa CBC unatekelezwa.

October 5, 2022