Familia ya aliyekuwa Waziri wa  elimu George Magoha, inapanga kuandaa msafara kwa heshima yake kabla ya mazishi yake yatakayoandaliwa jumamosi ijayo nyumbani kwake  Umiru Nyamninia kule Yala.

Kwa mujibu wa aliyekuwa katibu mkuu wa elimu ya msingi Julius Jwan ambaye ni msemaji wa familia yake,msafara huo utapitia maeneo yaliyokuwa na umuhimu kwa Magoha yakiwemo chuo cha sayansi ya kiafya katika chuo kikuu cha Nairobi,na makao makuu ya baraza la wauguzi na madakitari wa meno jijini Nairobi.

Jwan amesema msafara huo pia utapitia katika ubalozi wa Nigeria ,shule ya msingi ya St. George’s ,afisi za baraza la mitihani nchini kwenye barabara ya Dennis Pritt , shule ya upili ya State House Girls na ile ya Starehe Boys Centre alikosomea.

Mwili wa Magoha utawasili katika shule ya msingi ya Township Primary School, Yala saa saba mchana tarehe 10 mwezi huu kabla ya msafara utakaoelekea hadi shule ya upili ya  St Mary’s, Yala, na kisha ibaada ya misa takatifu ifuate nyumbani kwkae Umiru Nyamninia.

Ibada ya mazishi imeratibiwa kuandaliwa tarehe 11 katika chuo kikuu cha Odera Akang’o huko  Yala kuanzia saa nne asubuhi.

February 3, 2023