Gavana wa Kaunti ya Narok Patric Ntutu, mapema leo amezindua kituo cha kusaidia katika ukusanyaji wa ushuru mjini Narok, kituo ambacho kitawasaidia wananchi wa kaunti hii katika utekelezaji wa jukumu lao la kulipa ushuru.

Akizungumza katika kituo hicho, gavana Ntutu amesema kwamba kituo hiki kitasaidia katika kuimarisha jinsi ushuru unakusanywa katika kaunti ya narok na kusaidia katika kuimarisha miradi ya maendeleo kote katika kaunti hii.

Hafla hii iliandaliwa katika siku ambapo gavana Ntutu pia ameandaa hafla ya kuangazia uwajibikaji wa serikali yake mwaka mmoja tangu alipotwaa hatamu za uongozi. Gavana wa kaunti ya Vihiga Wilberforce Otichilo aliyehudhuria hafla hiyo amesema kaunti ya Narok ni kaunti ya kwanza nchini kufungua benki ya mapato.

Daktari Otichilo amesema hatua hiyo imefanya kaunti ya Narok kuwa miogoni mwa kaunti zilizopiga hatua kimaendeleo. Ametumia fursa hiyo kuwakumbusha wakazi wa Narok kumunga mkono gavana Ntutu ili aweze kutimiza ahadi zake kwa wananchi.

 

October 18, 2023