Idara ya Upelelezi wa Jinai DCI imemuamuru wakili Danstan Omari kufika kwenye makao makuu ya idara hiyo na kuandikisha taarifa kuhusiana na tuhuma za uvamizi wa polisi katika nyumba ya aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i.

Katika barua iliyoandikwa Februari 21, mpelelezi Michael K. Sang, amemueleza wakili huyo kufika katika makao makuu ya DCI Jumatano, Februari 22, bila kukosa.

Ofisa huyo amesema anachunguza tuhuma za uchapishaji wa Habari za Uongo kinyume na kifungu cha 23 cha Sheria ya Makosa ya Kompyuta na Makosa ya Mtandao ya mwaka 2018 pamoja na makosa mengine yanayohusiana na tuhuma za uvamizi.

Aidha Sang’ ameonya kuwa iwapo Omari atakosa kufika katika makao makuu ya DCI, basi  atashtakiwa.

February 21, 2023